Aliyekuwa bosi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ashtakiwa kwa Makosa Matano Likiwemo la Kutakatisha Fedha
Waliokuwa vigogo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) nchini Tanzania jana wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka matano yanayowakabili katika Namba 46 ya mwaka 2020.
Watuhumiwa hao waliofikishwa mahamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Laurien Bwanakunu na aliyekuwa Mkurugenzi wa Lojistiki wa MSD, Byekwaso Tabura.
Wakili wa Serikali, Faraji Nguka akiwasomea mashtaka washtakiwa hao, alidai kuwa kati ya Juai 1, 2016 na Juni 30, 2019 maeneo mbalimbali ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma, kwa pamoja walitengeneza genge la uhalifu kwa ajili ya kujipatia faida.
Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 20, 2019, washtakiwa wote kwa pamoja waliisababishia MSD hasara ya Sh 3,816,727,112.75.
Shtaka la tatu ambalo linamkabili Bwanakunu ni matumizi mabaya ya madaraka, ambapo inadaiwa kuwa kati ya Julai 1, 2916 na June 30, 2019 katika maeneo ya Keko wilaya ya Temeke mkoa wa Dar es Salaam, kwa makusudi alitumia nafasi yake kulipa kiasi cha Sh 3,816,727,112.75 kwa wafanyakazi wa MSD kama nyongeza ya mishahara na posho, bila ruhusa ya Katibu Mkuu Utumishi, na hivyo kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Katika shtaka la nne, washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 katika maeneo ya tofauti ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa pamoja waliruhusu uhifadhi mbaya wa vifaa tiba, uliosababisha vifaa hivyo kuharibika, hivyo kuisababishia MSD hasara ya Sh 85,199,879.65
Shtaka la tano linalowakabili washtakiwa hao ni utakatishaji fedha, ambapo inadaiwa kati ya Julai 1, 2016 na Juni 30, 2019 katika maeneo ya Keko Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam, wote kwa pamoja walijipatia Sh 1,603,991,095.37 wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu, ambao ni kuongoza genge la uhalifu.
Washtakiwa hao hawakurusiwa kujibu chochote, kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo. Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 18, 2020.
No comments