Alikotokea Robert Mugabe Na Alivyoingia GRACE Kwenye Ndoa Ya Robert Na Sally...
Afrika Hapo Zamani:
Ndugu zangu,
Ametokea wapi Robert Mugabe, mwana wa pili kati ya wana watatu wa baba yake, fundi Seremala wa kijijini, Mzee Mugabe?
Robert aliyezaliwa mwaka 1924 utotoni alikuwa mtulivu sana. Ndoto yake ilikuwa ama aje kuwa Mchungaji au Mwalimu wa shule.
Robert alishuhudia kaka yake Michael kwenye umri wa miaka 15, akifa kwa kula sumu ya majani wakiwa pamoja porini. Robert akabaki na mdogo wake tu.
Baba yake akaja kuitelekeza familia yao na Robert na mdogo wake wakalelewa na mama yao .
Hatimaye Robert akaja kuwa mwalimu kwenye shule ya msingi ya kijijini. Robert tangu utotoni alikuwa ni mwenye bidii ya masomo. Amefariki akiwa na digrii saba na tatu kati ya hizo amezipata akiwa gerezani, mojawapo ni ya sheria.
Alivyoingia Sally kwenye maisha ya Robert..
Robert alikutana na Sally alipokuwa akisoma Ghana. Walipendana na wakaoana mwaka 1961. Sally ni raia wa Ghana.
Waliamua kuishi wote Salisbury ( Sasa Harare). Robert akaingia matatani kisiasa na kufungwa mwaka 1964, kwa miaka kumi.
Mwaka mmoja kabla ya kifungo, walimzaa mwana wao pekee, Nhamodzenyika, ikiwa na maana ya nchi inayoteseka. Kwa kifupi walimwita Nhamo.
Sally ambaye alikuwa mcheshi na msomi alichangia sana kumjenga Robert hata kumsaidia kupata marafiki wa kuongea, maana, Robert ujanani alikuwa ni mkimya sana na asiyependa kujichanganya na watu.
Akiwa gerezani Zimbabwe, Sally alilazimika kukimbia Zimbabwe na kwenda kuishi kwao Ghana. Mwana wao Nhamo alifariki kwa malaria akiwa na miaka mitatu tu. Robert aliomba ruhusa ya bwana gereza ili akamzike mwanawe Ghana alikoishi Sally. Alikataliwa. Jambo hilo lilimhuzunisha sana Robert.
Mwaka 1974 Sally aliungana tena na Robert aliyetoka gerezani. Walikutana kwenye uwanja wa mapambano ya ukombozi kule Msumbiji.
Sally baada ya Uhuru wa Zimbabwe 1980, aliishi na mumewe Ikulu ya Harare. Sally alipendwa sana na Wazimbabwe. Wakazoea kumwita ' amai' ikiwa na maana ya mama yetu. Hata hii leo, Sally Mugabe anaonwa kama ' Mama wa Taifa' la Zimbabwe.
Alivyoingia Grace kwenye maisha ya Robert..
Grace Mafuru, msichana aliyeonekana mrembo aliyezaliwa Afrika Kusini, alifanya kazi ya Ukatibu Mukhtasi kwenye Ikulu ya Robert Mugabe. Ndipo hapo mahusiano ya kimapenzi kati ya Robert na Grace yakaanza huku Robert akiwa kwenye ndoa na Sally lakini wakiwa wapweke bila hata mtoto baada ya mwana wao Nhamo kufariki.
Grace akapata ujauzito wa Robert, 1988. Haikufanywa siri, Sally akajulishwa na akakubali hali hiyo mpya.
Mwaka 1992 Sally Mugabe alifariki kwa kuugua homa ya mapafu. Mwaka 1996 Robert na Grace wakafunga ndoa. Grace Mafuru akawa Grace Mugabe, First Lady.
Kuna ya kutafakari juu ya uongozi na mahusiano ya kimahaba. Wengi wanafikiri, kama angelikuwepo, kuwa Sally Mugabe angeliweza kumsaidia zaidi Robert Mugabe kiuongozi na pengine Robert Mugabe asingefikia hatua ya kung'ang'ania madaraka.
Kuna mengi pia ya kusimulia juu ya mahusiano ya Sally na Robert na namna Sally alivyomsaidia kumjenga Robert kisiasa katika ujana wao.
Kuna ya kusimulia pia, namna Grace alivyochangia kwenye anguko la Robert kisiasa.
Maggid Mjengwa.
Dar Es Salaam.
No comments