Hatimaye Siri Ya Diamond Kununua Mjengo Mpya Imevuja..Wasafi Kuhama Jengo
BAADA ya staa wa muziki barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kutangaza kununua mjengo mpya ambao ni hoteli ya nyota tatu iliyopo Mikocheni B jijini Dar, hatimaye siri ya kununua imevuja.
Hivi karibuni kupitia vyombo vyake vya habari vya Wasafi, Diamond au Mondi alitangaza kununua jumba hilo la Varlek Hotel na kusababisha maneno mengi kwa mashabiki wake wakijiuliza; ‘amewezaje kufanya kufuru hii kwenye kipindi cha janga la Corona?’
RISASI KAZINI
Baada ya tangazo hilo la Mondi, Gazeti la Risasi Jumamosi lilifunga safari hadi kwenye mjengo huo na kufanikiwa kuzungumza na baadhi ya watu waliokutwa hotelini hapo.
RISASI NA WAHUDUMU
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili ni wafanyakazi wa hoteli hiyo ambao walidai kuwa, Mondi alifikia hatua ya kununua mjengo huo ili ahamishie hapo makao makuu ya Kampuni ya Wasafi Ltd kuanzia studio za muziki za audio, video, ofisi za lebo, ofisi yake kuu na vyombo vyake vya habari vya Wasafi Radio na Wasafi TV.Makao makuu ya Wasafi kwa sasa yapo Kwazena, Mbezi-Beach jijini Dar.
Wahudumu hao walilitonya gazeti hili kuwa, Mondi aliamua hivyo baada ya mkataba wa mjengo aliopangisha pale Kwazena kukaribia ukingoni.Wengine walisema kuwa, Mondi anataka miradi yake yote iwe sehemu moja na kinachoonekana kwenye mjengo huo waliopo kwa sasa hautoshi, lakini huo alionunua ni mkubwa ambao unaweza kutumika kwa miradi yake yote.
ANATAKA KUHAMISHIA WASAFI
“Ni kweli Diamond amenunua mjengo huu, alikuja hapa kusaini makubaliano ya kuuziana.“Lakini nimesikia anataka kuibadilisha matumizi, haitakuwa hoteli tena kama ilivyo sasa.
“Nasikia anataka kuifanyia marekebisho kisha atahamishia makao makuu wa Wasafi hapa,” alisema mmoja wa wahudumu hao kwa ombi la kutotajwa gazetini.
RISASI LATINGA NDANI
Gazeti hili lilifanikiwa kuingia hadi ndani ya mjengo huo na kuwakuta wadada wawili ambao baada ya kujitambulisha na kuwaeleza nia ya kuwa mahali hapo, nao walikiri Mondi kununua mjengo huo.Walisema kuwa, hata wao wamesikia kuwa anataka kuhamishia mahali hapo studio za Wasafi.“Ni kweli Diamond amenunua hoteli hii, hivyo sisi tunasubiri tu kuambiwa tuondoke.“Lakini pia habari hizo za kuwa anataka kuhamishia studio zake hapa, sisi wenyewe tunazisikia kwa watu wengine ila hatuna uhakika sana.
“Kama mnavyoona, inatakiwa marekebisho hivyo inaweza kuwa kweli,” alisema mmoja wa wahudumu hao.Ili kupata ukweli wa ishu hiyo, gazeti hili lilimtafuta mmoja wa mameneja wa mwanamuziki huyo, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ ili azungumzie suala hilo, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.
MKUBWA FELA SASAIlibidi Risasi Jumamosi limtafute meneja wake mwingine ambaye ni Said Fela ‘Mkubwa Fela’ ambapo baada ya kupatikana hewani alisema kuwa, watu wasubiri mambo mazuri yanakuja na kila kitu kitawekwa wazi baadaye, lakini kwa sasa hana cha kuzungumza.
“Bado sijawa na jibu kamili kwa sasa hivi, kwa sababu pale panatakiwa pafanyiwe marekebisho na hao wanaofanya hivyo bado hawajamaliza ukarabati. Kwa hiyo, nikisema studio zinahamia pale, itakuwa ni uongo na nikisema hazihamii pale, utakuwa ni uongo vilevile.“Kwa nini msimpigie simu Nasibu (Mondi) mwenyewe mumsikie labda yeye ndiye anaweza akatoa ufafanuzi vizuri juu ya suala hilo,” alisema Mkubwa Fela.
Hata hivyo, Risasi lilipomtafuta Mondi, simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa, hivyo jitihada za kumpata zinaendelea
No comments