Naibu Waziri Aagiza Wafungwa Watumike Ujenzi wa Chuo cha Polisi Kurasini
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ameliekeza Jeshi la Polisi Tanzania kuwatumia wafungwa katika shughuli za ujenzi wa chuo cha polisi ili kupunguza gharama.
Masauni ametoa agizo hilo jana Jumanne Machi 12, 2019 alipotembelea majengo chakavu ya Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam ambayo yanatakiwa kurekebishwa kwa kutengenezwa mabweni na vyumba vya madarasa.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imeeleza kuwa Masauni amekwenda chuoni hapo kuangalia hatua za awali kabla ya kuanza kwa ujenzi huo na kupata mchanganuo wa kiasi cha Sh700 milioni zilizotolewa na Rais John Magufuli zitakavyotumika.
Kiasi hicho cha fedha kilichotolewa kwa polisi Machi 7, 2019 ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli aliyoitoa mwishoni mwa mwaka jana wakati wa mahafali ya kuhitimisha Mafunzo ya Kozi za Uofisa na Ukaguzi Msaidizi.
Masauni ameelekeza wafungwa wakitumika upo uwezekano wa kuokoa kiasi cha Sh200 milioni fedha ambazo zinaweza kutumika kwa matumizi mengine.
“Wizara ina taasisi ya magereza ambayo ina nguvu kazi ya kutosha, na Rais alishaagiza wafungwa watumike katika shughuli za uzalishaji, sioni sababu ya kutumia kiasi hicho cha pesa kuwalipa vibarua wa nje,” amesema.
“Naagiza muwasiliane na Jeshi la Magereza na kikosi cha ufundi kilichopo ndani ya Jeshi la Polisi ili muweze kuona ni vipi mnaokoa kiasi hicho,” amesema Masauni.
No comments